19
Paulo Huko Efeso
1 Apolo alipokuwa huko Korintho, Paulo alisafiri sehemu za bara, akafika Efeso. Huko akawakuta wanafunzi kadhaa,
2 akawauliza, “Je, mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini?”
Wakajibu, “Hapana, hata hatukusikia kuwa kuna Roho Mtakatifu.”
3 Ndipo Paulo akawauliza, “Je, mlibatizwa kwa ubatizo gani?” Wakajibu, “Kwa ubatizo wa Yohana.”
4 Paulo akasema, “Ubatizo wa Yohana ulikuwa wa toba, aliwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja baada yake, yaani, Yesu.”
5 Waliposikia haya, wakabatizwa katika jina la Bwana Yesu.
6 Paulo alipoweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akawashukia, nao wakanena kwa lugha mpya na kutabiri.
7 Walikuwa kama wanaume kumi na wawili.
8 Paulo akaingia katika sinagogi na kunena humo kwa ujasiri kwa muda wa miezi mitatu, akijadiliana na watu na kuwashawishi katika mambo ya Ufalme wa Mungu.
9 Lakini baadhi yao walikaidi. Walikataa kuamini, na wakakashifu ujumbe wake mbele ya umati wa watu. Basi Paulo aliachana nao. Akawachukua wanafunzi naye, akahojiana nao kila siku katika darasa la Tirano.
10 Jambo hili likaendelea kwa muda wa miaka miwili, kiasi kwamba Wayahudi na Wayunani wote walioishi huko Asia wakawa wamesikia neno la Bwana.
Wana Wa Skewa Wajaribu Kutoa Pepo Mchafu
11 Mungu akafanya miujiza mingi isiyo ya kawaida kwa mkono wa Paulo,
12 hivi kwamba leso au vitambaa vilivyokuwa vimegusa mwili wa Paulo viliwekwa juu ya wagonjwa, nao wakapona magonjwa yao, na pepo wachafu wakawatoka.
13 Basi baadhi ya Wayahudi wenye kutangatanga huku na huko wakitoa pepo wachafu wakajaribu kutumia jina la Bwana Yesu wale wenye pepo wakisema, “Kwa jina la Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo, nakuamuru utoke.”
14 Wana saba wa Skewa, Myahudi aliyekuwa kiongozi wa makuhani, walikuwa wanafanya hivyo.
15 Lakini pepo mchafu akawajibu, “Yesu namjua na Paulo pia namjua, lakini ninyi ni nani?”
16 Kisha yule mtu aliyekuwa na pepo mchafu akawarukia, akawashambulia vikali, akawashinda nguvu wote, wakatoka ndani ya ile nyumba wakikimbia wakiwa uchi na wenye majeraha.
17 Habari hii ikajulikana kwa Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawajaa wote, nalo jina la Bwana Yesu likaheshimiwa sana.
18 Wengi wa wale waliokuwa wameamini wakati huu wakaja na kutubu waziwazi kuhusu matendo yao maovu.
19 Idadi kubwa ya wale waliofanya mambo ya uganga wakaleta vitabu vyao na kuviteketeza kwa moto hadharani. Walipofanya hesabu ya thamani ya vitabu vilivyoteketezwa ilikuwa drakma 50,000 za fedha.
20 Hivyo neno la Bwana likaenea sana na kuwa na nguvu.
21 Baada ya mambo haya kutukia, Paulo akakusudia rohoni kwenda Yerusalemu kupitia Makedonia na Akaya. Akasema, “Baada ya kufika huko, yanipasa pia kwenda Rumi.”
22 Hivyo akatuma wasaidizi wake wawili, Timotheo na Erasto, waende Makedonia, wakati yeye mwenyewe alibaki kwa muda kidogo huko Asia.
Ghasia Huko Efeso
23 Wakati huo huo pakatokea dhiki kubwa kwa sababu ya Njia ile ya Bwana.
24 Mtu mmoja jina lake Demetrio mfua fedha aliyekuwa akitengeneza vinyago vya fedha vya Artemi na kuwapatia mafundi wake biashara kubwa,
25 aliwaita pamoja watu wengine waliofanya kazi ya ufundi kama yake na kusema, “Enyi watu, mnajua ya kuwa utajiri wetu unatokana na biashara hii!
26 Pia ninyi mmeona na kusikia jinsi ambavyo si huku Efeso peke yake lakini ni karibu Asia yote, huyu Paulo amewashawishi na kuvuta idadi kubwa ya watu kwa kusema kuwa miungu iliyotengenezwa na watu si miungu.
27 Kwa hiyo kuna hatari si kwa kazi yetu kudharauliwa tu, bali pia hata hekalu la mungu mke Artemi, aliye mkuu, anayeabudiwa Asia yote na ulimwengu wote, litakuwa limepokonywa fahari yake ya kiungu.”
28 Waliposikia maneno haya, wakaghadhibika, wakaanza kupiga kelele, “Artemi wa Waefeso ni mkuu!”
29 Mara mji wote ukajaa ghasia. Wakawakamata Gayo na Aristarko, watu wa Makedonia waliokuwa wakisafiri pamoja na Paulo, na watu wakakimbilia katika ukumbi wa michezo kama mtu mmoja.
30 Paulo akataka kuingia katikati ya umati huo, lakini wanafunzi hawakumruhusu.
31 Hata baadhi ya viongozi wa sehemu ile, waliokuwa rafiki zake Paulo, wakatuma watu wakitamani asiingie katika ule ukumbi.
32 Ule umati ulikuwa na taharuki. Wengine walikuwa wakipiga kelele, hawa wakisema hili na wengine lile. Idadi kubwa ya watu hawakujua hata ni kwa nini walikuwa wamekusanyika huko.
33 Wayahudi wakamsukumia Aleksanda mbele na baadhi ya watu kwenye ule umati wakampa maelekezo. Akawaashiria kwa mkono ili watulie aweze kujitetea mbele ya watu.
34 Lakini walipotambua kwamba alikuwa Myahudi, wote wakapiga kelele kwa sauti moja kwa karibu muda wa saa mbili, wakisema, “Artemi wa Efeso ni mkuu!”
35 Baadaye karani wa mji akaunyamazisha ule umati wa watu na kusema, “Enyi watu wa Efeso, je, ulimwengu wote haujui ya kuwa mji wa Efeso ndio unaotunza hekalu la Artemi aliye mkuu na ile sanamu yake iliyoanguka kutoka mbinguni?
36 Kwa hiyo, kwa kuwa mambo haya hayakanushiki, inawapasa mnyamaze na wala msifanye lolote kwa haraka.
37 Kwa kuwa mmewaleta hawa watu hapa, ingawa hawajaiba hekaluni wala kumkufuru huyu mungu wetu wa kike.
38 Basi, ikiwa Demetrio na mafundi wenzake wana jambo zito dhidi ya mtu yeyote, mahakama ziko wazi na wasaidizi wa mwakilishi wa mtawala. Wanaweza kufungua mashtaka.
39 Lakini kama kuna jambo jingine lolote zaidi mnalotaka kulileta, itabidi lisuluhishwe katika kusanyiko halali.
40 Kama ilivyo sasa, tuko hatarini kushtakiwa kwa kufanya ghasia kwa sababu ya tukio la leo. Kwa kuwa hakuna sababu tutakayoweza kutoa kuhalalisha msukosuko huu.”
41 Baada ya kusema haya akavunja mkutano.