17
Yesu Afundisha Kuhusu Majaribu, Dhambi Na Imani
(Mathayo 18:6-7, 21-22; Marko 9:42)
1 Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Mambo yanayosababisha watu watende dhambi hayana budi kutukia. Lakini ole wake mtu yule anayeyasababisha.
2 Ingekuwa heri kama mtu huyo angefungiwa jiwe la kusagia shingoni na kutoswa baharini, kuliko kumsababisha mmojawapo wa hawa wadogo kutenda dhambi.
3 Kwa hiyo, jilindeni.
“Kama ndugu yako akikukosea mwonye, naye akitubu, msamehe.
4 Kama akikukosea mara saba kwa siku moja na mara saba kwa siku moja akaja kwako akisema, ‘Ninatubu,’ msamehe.”
Imani
5 Mitume wake wakamwambia Bwana, “Tuongezee imani.”
6 Bwana akawajibu, “Kama mkiwa na imani ndogo kama punje ya haradali, mngeweza kuuambia mti huu wa mkuyu, ‘Ngʼoka ukaote baharini,’ nao ungewatii.
Wajibu Wa Mtumishi
7 “Ikiwa mmoja wenu ana mtumishi anayelima shambani au anayechunga kondoo, je, mtumishi huyo arudipo atamwambia, ‘Karibu hapa keti ule chakula?’
8 Je, badala yake, hatamwambia, ‘Niandalie chakula, nile, jifunge unitumikie ninapokula na kunywa; baadaye waweza kula na kunywa?’
9 Je, huyo mtu atamshukuru mtumishi huyo kwa kutimiza yale aliyoamriwa?
10 Vivyo hivyo nanyi mkiisha kufanya mliyoagizwa, semeni, ‘Sisi tu watumishi tusiostahili; tumefanya tu yale tuliyopaswa kufanya.’ ”
Yesu Atakasa Wakoma Kumi
11 Yesu alipokuwa njiani akienda Yerusalemu, alipitia mpakani mwa Samaria na Galilaya.
12 Alipokuwa akiingia kwenye kijiji kimoja, watu kumi waliokuwa na ukoma wakakutana naye. Wakasimama mbali,
13 wakapaza sauti, wakasema, “Yesu, Bwana, tuhurumie!”
14 Alipowaona akawaambia, “Nendeni mkajionyeshe kwa makuhani.” Nao walipokuwa njiani wakienda, wakatakasika.
15 Mmoja wao alipoona kwamba amepona, akarudi kwa Yesu, akimsifu Mungu kwa sauti kuu.
16 Akajitupa miguuni mwa Yesu akamshukuru. Yeye alikuwa Msamaria.
17 Yesu akauliza, “Je, hawakutakaswa wote kumi? Wako wapi wale wengine tisa?
18 Hakuna hata mmoja aliyeonekana kurudi ili kumshukuru Mungu isipokuwa huyu mgeni?”
19 Yesu akamwambia, “Inuka na uende zako, imani yako imekuponya.”
Kuja Kwa Ufalme Wa Mungu
(Mathayo 24:23-28, 37-41)
20 Yesu alipoulizwa na Mafarisayo Ufalme wa Mungu utakuja lini, yeye akawajibu, “Ufalme wa Mungu hauji kwa kuchunguza kwa bidii,
21 wala watu hawatasema, ‘Huu hapa,’ au ‘Ule kule,’ kwa maana Ufalme wa Mungu umo ndani yenu.”
22 Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Wakati utafika ambapo mtatamani kuiona moja ya siku ya Mwana wa Adamu, lakini hamtaiona.
23 Watu watawaambia, ‘Yule kule!’ Au, ‘Huyu hapa!’ Msiwakimbilie.
24 Kwa maana kama vile umeme wa radi umulikavyo katika anga kuanzia mwisho mmoja hadi mwingine, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu katika siku yake.
25 Lakini kwanza itampasa kuteseka katika mambo mengi na kukataliwa na kizazi hiki.
26 “Kama ilivyokuwa siku za Noa, ndivyo itakavyokuwa katika siku za Mwana wa Adamu.
27 Watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka siku ile Noa alipoingia katika safina. Ndipo gharika ikaja na kuwaangamiza wote.
28 “Ndivyo ilivyokuwa katika siku za Loti: Watu walikuwa wakila na kunywa, wakinunua na kuuza, wakilima na kujenga.
29 Lakini siku ile Loti alipoondoka Sodoma, ikanyesha mvua ya moto na kiberiti kutoka mbinguni ukawaangamiza wote.
30 “Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile Mwana wa Adamu atakapofunuliwa.
31 Siku hiyo, mtu yeyote aliye juu ya dari ya nyumba yake, hata vitu vyake vikiwa ndani ya hiyo nyumba, asishuke kuvichukua. Vivyo hivyo mtu aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua chochote.
32 Mkumbukeni mke wa Loti!
33 Mtu yeyote anayejaribu kuyaokoa maisha yake atayapoteza, na yeyote atakayeyapoteza maisha yake atayaokoa.
34 Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa wamelala kitanda kimoja; naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa.
35 Wanawake wawili watakuwa wanasaga nafaka pamoja; naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa. [
36 Wanaume wawili watakuwa wanafanya kazi pamoja shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.]”
37 Kisha wakamuuliza, “Haya yatatukia wapi Bwana?”
Akawaambia, “Pale ulipo mzoga, huko ndiko tai watakapokusanyika.”