21
Sadaka Ya Mjane
(Marko 12:41-44)
Yesu alipoinua macho yake, aliwaona matajiri wakiweka sadaka zao kwenye sanduku la hazina ya Hekalu. Akamwona pia mjane mmoja maskini akiweka humo sarafu mbili ndogo za shaba. Yesu akasema, “Amin, nawaambia, huyu mjane maskini ameweka humo zaidi ya watu wengine wote. Hawa watu wengine wote wametoa sadaka kutokana na wingi wa mali zao. Lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake vyote alivyokuwa navyo, hata kile alichohitaji ili kuishi.”
Dalili Za Siku Za Mwisho
(Mathayo 24:1-2; Marko 13:1-2)
Baadhi ya wanafunzi wake wakawa wanamwonyesha jinsi Hekalu lilivyopambwa kwa mawe mazuri na kwa vitu vilivyotolewa kuwa sadaka kwa Mungu. Lakini Yesu akawaambia, “Kuhusu haya mnayoyaona hapa, wakati utafika ambapo hakuna jiwe moja litakalobaki juu ya jingine, bali kila moja litabomolewa.”
Mateso
(Mathayo 24:3-14; Marko 13:3-13)
Wakamuuliza, “Mwalimu, mambo haya yatatukia lini? Ni dalili gani itaonyesha kwamba yanakaribia kutendeka?”
Yesu akawajibu, “Jihadharini msije mkadanganywa. Maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye,’ na, ‘Wakati umekaribia.’ Msiwafuate. Lakini msikiapo habari za vita na machafuko, msiogope. Kwa maana hayo ni lazima yatokee kwanza, ila ule mwisho hautakuja wakati huo.”
10 Kisha akawaambia: “Taifa litainuka dhidi ya taifa jingine, na ufalme mmoja dhidi ya ufalme mwingine. 11 Kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi, na njaa kali, na magonjwa ya kuambukiza katika sehemu mbalimbali. Pia kutakuwa na matukio ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni.
12 “Lakini kabla yote hayajatokea, watawakamata ninyi na kuwatesa. Watawatia mikononi mwa wakuu wa masinagogi na kuwafunga magerezani. Nanyi mtapelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya Jina langu. 13 Hii itawapa nafasi ya kushuhudia. 14 Lakini kusudieni mioyoni mwenu msisumbuke awali kuhusu mtakalosema mbele ya mashtaka. 15 Kwa maana nitawapa maneno na hekima ambayo hakuna hata adui yenu mmoja atakayeweza kushindana nayo wala kuipinga. 16 Mtasalitiwa hata na wazazi, ndugu, jamaa na marafiki, na baadhi yenu watawaua. 17 Mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya Jina langu. 18 Lakini hapatakuwa na unywele mmoja wa kichwa chenu utakaoangamia. 19 Kwa kuvumilia mtaokoa roho zenu.
Kuharibiwa Kwa Yerusalemu Kwatabiriwa
(Mathayo 24:15-21; Marko 13:14-19)
20 “Mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, basi fahamuni kwamba kuharibiwa kwake kumekaribia. 21 Wakati huo, wale walio Uyahudi wakimbilie milimani, walio mjini Yerusalemu watoke humo, nao wale walioko mashambani wasiingie mjini. 22 Kwa sababu huu utakuwa ni wakati wa adhabu ili kutimiza yote yaliyoandikwa. 23 Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo! Kutakuwa na dhiki kuu katika nchi na ghadhabu juu ya hawa watu. 24 Wataanguka kwa makali ya upanga, na wengine watachukuliwa kuwa mateka katika mataifa yote. Nao mji wa Yerusalemu utakanyagwa na watu wa Mataifa hadi muda wa hao watu wa Mataifa utimie.
Kuja Kwa Mwana Wa Adamu
(Mathayo 24:29-35; Marko 13:24-31)
25 “Kutakuwa na ishara katika jua, mwezi na nyota. Hapa duniani, mataifa yatakuwa katika dhiki na fadhaa kutokana na ngurumo na misukosuko ya bahari. 26 Watu watazimia roho kutokana na hofu kuu na kuyaona yale mambo yanayotokea duniani, kwa maana nguvu za angani zitatikisika. 27 Wakati huo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni pamoja na uweza na utukufu mkuu. 28 Mambo haya yatakapoanza kutendeka, simameni na mkaviinue vichwa vyenu, kwa sababu ukombozi wenu umekaribia.”
29 Akawaambia mfano huu: “Uangalieni mtini na miti mingine yote. 30 Inapochipua majani, ninyi wenyewe mnaweza kuona na kutambua wenyewe ya kuwa wakati wa kiangazi umekaribia. 31 Vivyo hivyo, myaonapo mambo haya yakitukia, mnatambua kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.
32 “Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia. 33 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.”
Siku Ya Mwisho Itakuja Ghafula
34 “Jihadharini mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na fadhaa za maisha haya, nayo siku ile ikawakuta ninyi bila kutazamia kama vile mtego unasavyo. 35 Kwa maana kama vile mtego unasavyo, ndivyo siku hiyo itakavyowapata wanadamu wote waishio katika uso wa dunia yote. 36 Kesheni daima na mwombe ili mweze kuokoka na yale yote yatakayotokea na kusimama mbele ya Mwana wa Adamu.”
37 Kila siku Yesu alikuwa akifundisha Hekaluni, na jioni ilipofika, alikwenda zake kwenye Mlima wa Mizeituni na kukaa huko usiku kucha. 38 Nao watu wote walikuja asubuhi na mapema Hekaluni ili kumsikiliza.