24
1 Mwanamume akimchukua mke na kumuoa, na mke asipokubalika machoni pa mumewe kwa sababu kagundua jambo ambalo si jema kwake, basi anatakiwa amwandikie talaka, aiweke mkononi mwake, na kumfukuza nyumbani kwake.
2 Akishaondoka nyumbani kwake, anaweza kwenda na kuwa mke wa mwanamume mwingine.
3 Iwapo mume wa pili akamchukia na kumwandikia talaka, akaiweka mkononi mwake, na kumfukuza nyumbani kwake; au huyu mume wa pili akafariki, mwanamume aliyemchukua kuwa mke wake –
4 basi mume wa awali, yule aliyemfukuza mara ya kwanza, haruhusiwi kumchukua tena awe mke wake, baada ya yeye kuwa mchafu, kwa maana hiyo itakuwa ni chukizo kwa Yahwe. Hautakiwi kusababisha nchi iwe na hatia, nchi ambayo Yahwe Mungu wako anakupatia kama urithi.
5 Mwanamume atakapochukua mke mpya, hatakwenda vitani na jeshi, na wala hataamrishwa kwenda kwenye shughuli yoyote ya kulazimishwa; atakuwa huru kuwa nyumbani kwa mwaka mzima na atamfurahisha mke wake aliyemchukua.
6 Mwanamume yeyote hatachukua kinu wala jiwe la kinu kama dhamana, kwa maana hivyo itakuwa kuchukua Maisha ya mtu kama dhamana.
7 Iwapo mwanamume kakutwa kamteka mmoja wa kaka zake miongoni mwa watu wa Israeli, na kumtendea kama mtumwa na kisha kumuuza, huyo mwizi lazima afe; na utakuwa umeondoa uovu miongoni mwenu.
8 Kuwa mwangalifu kuhusu kiini chochote cha ukoma, ili kwamba uwe makini katika kuchunguza na kufuata kila agizo linalopewa kwako ambalo makuhani, Walawi, wanakufundisha; kama nilivyowaamuru, ili utekeleze.
9 Kumbukeni nini Yahwe Mungu wako alichomfanya Miriam ulipokuwa ukitoka Misri.
10 Utoapo mkopo wa aina yoyote kwa jirani yako, hautakiwi kwenda ndani ya nyumba yake kutafuta dhamana yake.
11 Utasimama nje, na mwanamume aliyekopa kwako ataleta dhamana yake nje kwako.
12 Iwapo ni mtu maskini, hautakiwi kulala na dhamana yake ikiwa mikononi mwako.
13 Hakika unapaswa kumrejeshea dhamana yake kabla jua halijazama, ili aweze kulala ndani ya vazi lake na akubariki; itakuwa utakatifu kwako mbele za Yahwe Mungu wako.
14 Hautakiwi kumuonea mtumishi wa kuajiriwa ambaye ni maskini na mhitaji, hata kama ni jamaa wa Israeli, au ni kati ya wageni mbao wamo katika nchi ndani ya malango ya mji wako;
15 Kila siku unapaswa kumlipa mshahara wake; jua halipaswi kuzama kabla ya suala hili kutatuliwa, kwa maana ni maskini na anautegemea. Fanya hivi ili asilie dhidi yako kwa Yahwe, na kwamba isiwe ikawa dhambi ambayo umeitenda.
16 Wazazi hawapaswi kuuwawa kwa niaba ya watoto wao, na wala watoto hawapaswi kuuawa kwa niaba ya wazazi wao. Badala yake, kila mtu anapaswa kuuwawa kwa dhambi yake mwenyewe.
17 Haupaswi kutumia nguvu kuchukua haki inayomhusu mgeni au yatima, wala kuchukua vazi la mjane kama dhamana.
18 Badala yake, unapaswa ukumbuke ya kwamba ulikuwa mtumwa Misri, na kwamba Yahwe Mungu wako alikukomboa kutoka kule. Kwa hiyo ninakuagiza kutii amri hii.
19 Utakapovuna zao lako shambani mwako, na ukasahau kipande cha mbegu shambani, haupaswi kurudi na kukichukua; kinapaswa kuwa cha mgeni, cha yatima, au cha mjane, ili Yahwe Mungu wako akubariki katika kazi ya mikono yako.
20 Utakapotikisa mti wako wa mzeituni, haupaswi kupanda juu ya matawi tena; itakuwa kwa ajili ya mgeni, kwa yatima na kwa mjane.
21 Utakapokusanya mizabibu shambani mwako, haupaswi kukusanya masazo yake tena. Kinachobaki kitakuwa cha mgeni, cha yatima na cha mjane.
22 Unatakiwa ukumbuke kuwa ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri; kwa hiyo nakuagiza kutii amri hii.