2
1 Watoto wangu wapendwa, nawaandikia mambo haya kwenu ili msitende dhambi. Lakini kama mmoja wenu akitenda dhambi, tunaye wakili aliye pamoja na Baba, Yesu Kristo- ambaye ni mwenye haki.
2 Yeye ni mpatanishi kwa dhambi zetu, na si kwa dhambi zetu pekee, lakini pia kwa ulimwengu mzima.
3 Kwa hili twajua kwamba twamjua yeye, kama tukizitunza amri zake.
4 Yeye asemaye, “Namjua Mungu,” lakini hazishiki amri zake, ni mwongo, na kweli haimo ndani yake.
5 Lakini yeyote ashikaye neno lake, kweli katika mtu yule upendo wa Mungu umekamilishwa. Katika hili twajua kwamba tuko ndani yake.
6 Yeye asemaye anaishi ndani ya Mungu anapaswa mwenyewe pia kuenenda kama vile Yesu Kristo alivyoenenda.
7 Wapenzi, siwaandikii ninyi amri mpya, bali amri ya zamani ambayo mmekwisha kuwa nayo tangu mwanzo. Amri ya zamani ni neno ambalo mlilolisikia.
8 Hata hivyo ninawaandikia ninyi amri mpya, ambayo ni kweli katika Kristo na kwenu, kwa sababu giza linapita, na nuru ya kweli iko tayari inaangaza
9 Yeye asemeye yuko kwenye nuru na amchukia ndugu yake yuko katika giza hata sasa.
10 Yeye ampendaye ndugu yake anaishi katika nuru na hakuna jambo lolote liwezalo kumkwaza.
11 Lakini yeye amchukiaye ndugu yake yuko gizani na anatembea gizani; Yeye hajui wapi aendako, kwa sababu giza limeyapofusha macho yake.
12 Nawaandikia ninyi, watoto wapendwa, kwa sababu mmesamehewa dhambi zenu kwa ajili ya jina lake.
13 Nawaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mnamjua yeye aliye tangu mwanzo. Nawaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mmemshinda yule mwovu. Nimewaandikia ninyi, watoto wadogo, kwa sababu mnamjua Baba.
14 Nimewaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mnamjua yeye aliye tangu mwanzo. Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mko imara, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, na mmemshinda yule mwovu.
15 Msiipende dunia wala mambo ambayo yaliyo katika dunia. Iwapo yule ataipenda dunia, upendo wa kumpenda Baba haumo ndani yake.
16 Kwani kila kitu kilichomo katika dunia- tamaa ya mwili, tamaa ya macho, na kiburi cha uzima- havitokani na Baba lakini vinatokana na dunia.
17 Dunia na tamaa zake zinapita. Bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu huyo adumu milele.
18 Watoto wadogo, ni wakati wa mwisho. Kama ambavyo mmesikia kwamba mpinga kristo anakuja, hata sasa wapinga kristo wamekuja, kwa hali hii tunajua kwamba ni wakati wa mwisho.
19 Walikwenda zao kutoka kwetu, kwani hawakuwa wa kwetu. Kama vile wangekuwa wa kwetu wangeendelea kuwa pamoja nasi. Lakini wakati walipo kwenda zao, hicho kilionyesha hawakuwa wa kwetu.
20 Lakini mumetiwa mafuta na yule Mtakatifu, nanyi nyote mnaijua kweli.
21 Sikuwaandikia ninyi kwa sababu hamuijui kweli, bali kwa sababu mnaijua na kwa sababu hakuna uongo wa ile kweli
22 Nani ni mwongo bali ni yeye anayepinga kwamba Yesu ni Kristo? Huyu mtu ni mpinga kristo, pale anapo mpinga Baba na Mwana.
23 Hakuna anaye mpinga Mwana akawa na Baba. Yeyote anaye mkiri Mwana anaye Baba pia.
24 Kama kwa ajili yenu, kile mlichosikia toka mwanzo acha kiendelee kuwa ndani yenu. Kama kile mlichosikia toka mwanzo kitakaa ndani yenu, pia, mtakaa ndani ya Mwana na Baba.
25 Na hii ni ahadi aliyotupatia sisi: uzima wa milele.
26 Nimewaandikia haya ninyi kuhusu wale ambao wangewaongoza ninyi katika upotevu.
27 Na kwa ajili yenu, yale mafuta mliyoyapokea kutoka kwake yanakaa ndani yenu, na hamtahitaji mtu yeyote kuwafundisha. bali kama mafuta yake yanawafundisha kuhusu mambo yote na ni kweli na siyo uongo, na hata kama yameshawafundisha, kaeni ndani yake.
28 Na sasa, watoto wapendwa, kaeni ndani yake, ili wakati atakapotokea, tuweze kuwa na ujasiri na siyo kujisikia aibu mbele yake katika kuja kwake.
29 Kama mnajua kuwa yeye ni mwenye haki, mnajua kwamba kila mmoja atendaye haki amezaliwa na yeye.