3
1 Oneni ni pendo la namna gani ametupatia Baba, kwamba tunaitwa watoto wa Mungu, na hivi ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui kwa kuwa haukumtambua yeye.
2 Wapendwa sisi sasa ni watoto wa Mungu, na haijadhihirika bado jinsi tutakavyokuwa. Twajua kwamba Kristo atakapoonekana, tutafanana naye, kwani tutamuona kama alivyo.
3 Na kila mmoja ambaye ana ujasiri huu kuhusu wakati ujao ulioelekezwa kwake, hujitakasa mwenyewe kama yeye alivyo mtakatifu.
4 Kila mtu anayeendelea kutenda dhambi huvunja sheria. Kwa sababu dhambi ni uvunjaji sheria.
5 Mnajua Kristo alidhihilishwa ili kuziondoa dhambi kabisa. Na ndani yake hamna dhambi.
6 Hakuna hata mmoja adumue ndani yake na kuendelea kutenda dhambi. Hakuna mtu hata mmoja adumuye katika dhambi ikiwa amemuona au kumfahamu yeye.
7 Watoto wapendwa, msikubali kupotoshwa na mtu yeyote. Atendaye haki ni mwenye haki, kama vile Kristo naye alivyo mwenye haki.
8 Atendaye dhambi ni wa ibilisi, kwa sababu ibilisi ni mtenda dhambi tangu mwanzo. Kwa sababu hii Mwana wa Mungu alidhihilishwa ili aweze kuziharibu kazi za ibilisi.
9 Yeyote aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu mbegu ya Mungu hukaa ndani yake. Hawezi kuendelea kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa na Mungu.
10 Katika hili watoto wa Mungu na watoto wa ibilisi wanafahamika. Yeyote asiyetenda kilicho cha haki, siyo wa Mungu, wala yule ambaye hawezi kumpenda ndugu yake.
11 Kwani huu ndio ujumbe mliousikia kutoka mwanzo, kwamba tunapaswa kupendana sisi kwa sisi,
12 siyo kama Kaini ambaye alikuwa wa mwovu na alimuua ndugu yake. Na kwa nini alimuua? Kwa sababu matendo yake yalikuwa maovu, na yale ya ndugu yake yalikuwa ya haki.
13 Ndugu zangu, msishangae, endapo ulimwengu utawachukia.
14 Twajua tumekwisha toka mautini na kuingia uzimani, kwa sababu tunawapenda ndugu. Yeyote ambaye hana upendo hudumu katika mauti.
15 Mtu yeyote anaye mchukia ndugu yake ni muuaji. Na mnajua kuwa uzima wa milele haukai ndani ya muuaji.
16 Katika hili tunalijua pendo, kwa sababu kristo aliutoa uhai wake kwa ajili yetu. Nasi yatupasa kuyatoa maisha yetu kwa ajili ya ndugu.
17 Lakini yeyote aliye na vitu, na anamuona ndugu yake mwenye uhitaji, lakini huuzuia moyo wake wa huruma kwa ajili yake; je, upendo wa Mungu unakaaje ndani yake?
18 Watoto wangu wapenzi, tusipende kwa midomo wala kwa maneno matupu bali katika vitendo na kweli.
19 Katika hili tunajua kwamba sisi tuko katika kweli, na mioyo yetu inathibitika katika yeye.
20 Ikiwa kama mioyo yetu yatuhukumu, Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu, na yeye hujua mambo yote.
21 Wapenzi, kama mioyo yetu haituhukumu, tunao ujasiri kwa Mungu.
22 Na chochote tuombacho tutakipokea kutoka kwake, kwa sababu tunazishika amri zake na tunafanya mambo yanayopendeza mbele zake.
23 Na hii ndiyo amri yake- ya kwamba yatupasa kuamini katika jina la Mwanaye Yesu Kristo na kupendana sisi kwa sisi-kama alivyotupatia amri yake.
24 Anayezitii amri zake hudumu ndani yake, na Mungu hukaa ndani yake. Na kwa sababu hii twajua kuwa hukaa ndani yetu, Kwa yule Roho aliyetupa.