4
1 Baada ya mambo haya nilitazama, nikaona kuwa mlango ulikuwa umefunguliwa mbinguni. Ile sauti ya kwanza, ikizungumza nami kama tarumbeta, ikisema, “Njoo hapa, nitakuonesha yatakayotokea baada ya mambo haya.”
2 Mara moja nilikuwa katika Roho, niliona kulikuwa na kiti cha enzi kimewekwa mbinguni, na mtu amekikalia.
3 Mmoja aliyekuwa amekikalia alionekana kama jiwe la yaspi na akiki. Kulikuwa na upinde wa mvua umekizunguka kiti cha enzi. Upinde wa mvua ulionekana kama zumaridi.
4 Kukizunguka kiti cha enzi kulikuwa na viti vya enzi vingine ishirini na vinne, na waliokaa kwenye viti vya enzi walikuwa wazee ishirini na wanne, wamevikwa mavazi meupe na taji za dhahabu vichwani mwao.
5 Kutoka katika kiti cha enzi kulitoka miale ya radi, muungurumo na radi. Taa saba zilikuwa zikiwaka mbele ya kiti cha enzi, taa ambazo ni roho saba za Mungu.
6 Tena mbele ya kiti cha enzi kulikuwa na bahari, iliyowazi kama kioo. Wote kuzunguka kiti cha enzi kulikuwa na wenye uhai wanne, waliojaa macho mbele na nyuma.
7 Kiumbe wa kwanza mwenye uhai alikuwa kama simba, kiumbe wa pili mwenye uhai alikuwa kama ndama, kiumbe wa tatu mwenye uhai alikuwa na uso kama wa mwanadamu, na yule mwenye uhai wa nne alikuwa kama tai apaaye.
8 Viumbe wenye uhai wanne kila mmoja alikuwa na mabawa sita, wamejaa macho juu na chini yake. Usiku na mchana hawakomi kusema, “Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu ni Bwana Mungu, mtawala juu ya wote, aliyekuwepo, na aliyepo na atakayekuja.”
9 Kila wakati viumbe wenye uhai walipotoa utukufu, heshima, na kushukuru mbele za aliyekuwa ameketi kwenye hicho kiti cha enzi, yeye aishiye milele na daima,
10 wazee ishirini na wanne walisujudu wenyewe mbele yake aliyekikalia kiti cha enzi. Waliinama chini kwake aishiye milele na daima na kutupa chini taji zao mbele ya kiti cha enzi wakisema,
11 “Wastahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, kupokea utukufu na heshima na nguvu. Kwa kuwa uliviumba vitu vyote, na kwa mapenzi yako, vilikuwepo na viliumbwa.”