5
1 Kisha nikaona katika mkono wa kulia wa yule aliyekuwa amekaa katika kiti cha enzi, gombo lililoandikwa mbele na nyuma, na lilikuwa limetiwa mihuri saba.
2 Nilimwona malaika mwenye nguvu akihubiri kwa sauti kubwa, “Nani astahiliye kulifungua gombo na kuzivunja mihuri yake?”
3 Hakuna mtu mbinguni au duniani au chini ya dunia aliyeweza kulifungua gombo au kulisoma.
4 Nililia kwa uchungu kwa kuwa hakupatikana yeyote aliyestahili kulifungua gombo au kulisoma.
5 Lakini mmoja wa wazee akaniambia, “Usilie. Tazama! Simba wa kabila ya Yuda, shina la Daudi, ameshinda, na anaweza kulifungua gombo na mihuri yake saba.”
6 Kati ya kiti cha enzi na wenye uhai wanne na miongoni mwa wazee, niliona mwanakondoo amesimama, akionekana kama aliye uawa. Alikuwa na pembe saba na macho saba - hizi ni roho saba za Mungu zilizotumwa duniani kote.
7 Akaenda akalichukua gombo kutoka katika mkono wa kuume wa yule aliye kaa katika kiti cha enzi.
8 Alipolichukua gombo, wenye uhai wanne na wazee ishirini na wanne wakainama hadi nchi mbele ya mwanakondoo. Kila mmoja alikuwa na kinubi na bakuli ya dhahabu iliyojaa uvumba ambayo ni maombi ya waamini.
9 Waliimba wimbo mpya: “Unastahili kulitwaa gombo na kuzifungua muhuri zake. Kwa kuwa ulichinjwa, na kwa damu yako ukamnunulia Mungu watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa.
10 Ukawafanya ufalme na makuhani kwa ajili ya kumtumikia Mungu wetu, nao watatawala juu ya nchi.”
11 Kisha nilitazama na nikasikia sauti ya malaika wengi kuzunguka kiti cha enzi - idadi yao ilikuwa 200, 000, 000 na wenye uhai na wazee.
12 Wakasema kwa sauti kuu, “Astahili mwanakondoo ambaye amechinjwa kupokea uwezo, utajiri, hekima, nguvu, heshima, utukufu, na sifa.”
13 Nikasikia kila kilichoumbwa kilichokuwa mbinguni na duniani na chini ya nchi na juu ya bahari, kila kitu ndani yake kikisema, “Kwake yeye aketiye juu ya kiti cha enzi na kwa mwanakondoo, kuwe sifa, heshima, utukufu na nguvu ya kutawala milele na milele.”
14 Wenye uhai wanne wakasema, “Amina!” na wazee wakainama chini na kuabudu.